KIBAHA, TANZANIA
Timu ya Soka ya Kanda ya Zanzibar imefanikiwa kutwaa ubingwa wa michuano ya 34 ya Umoja wa Michezo na Sanaa kwa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) kwa kuifunga Kanda ya Kaskazini Mashariki kwa magoli 2-1.
Fainali hiyo ambayo ilikuwa na msisimko tangu mwanzao wa mchezo na kushuhudiwa na mgeni rasmi Naibu Waziri wa Sheria na Katiba Anjela Kairuki, ilipigwa kwenye uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha.
Zanzibar walianza kuandika bao kwenye dakika ya 56 ya mchezo kupitia kwa Ibrahim Hamad ambaye aliongeza bao la pili kwenye dakika ya 61 ya mchezo huo ambao uliwavutia wakazi wa mji wa Kibaha na vitongoji vyake.
Kaskazini Mashariki walijitahidi kuhakikisha wanarejesha magoli hayo lakini ukuta wa Zanzibar ulikuwa imara na kuondo hatari zote zilizoelekezwa langoni mwao kabla ya dakika ya 80 kupata bao kupitia kwa Obisa Joel.
Kwa upande wa wasichana Kanda ya Dar es Salaam walifanikiwa kutwaa ubingwa baada ya kuifunga Kanda ya Mashariki kwa penati 3-1 baada ya dakika 90 kuisha timu hizo zikiwa sare ya goli 1-1.
Kwenye mchezo wa Kikapu wavulana Dar es Salaam iliifunga Mashariki kwa vikapu 88-72. Kutokana na matokeo ya michezo mbalimbali Kanda ya Dar es Salaam wameteuliwa kuwa mabingwa wa jumla wakifuatiwa na wenyeji Mashariki na watatu ni kanda ya Kaskazini Magharibi.
Michezo hiyo ya 34 iliwashirikisha wanamichezo 1,659 kutoka kanda 12 na walishindana kwenye michezo ya bao, soka, meza, kikapu, riadha, mikono na wavu.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Sheria na Katiba Anjelina Kairuki amesema kuwa kamati ya bunge ya sheria itafuatilia halmashauri ambazo zitashindwa kutekeleza agizo la serikali la kutenga bajeti za michezo.
Akifungua mashindano ya 34 ya Umoja wa Michezo na Sanaa kwa Shule za Sekondari (UMISSETA) kwenye uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha,mkoa wa Pwani, alisema, serikali imekuwa ikitoa maelekezo kwa halmashauri kuweka mipango na kupanga bajeti kwa ajili ya kuendeleza michezo hasa ya vijana wadogo lakini utekelezaji imekuwa ni tatizo.
“Kamati ya hseria na katiba ipo hivyo tungependa yaleyanayopendekezwa yafanywe kwa vitendo kwani tunaweza kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira kupitia michezo,” alisema Kairuki.
Alisema kuwa ili nchi iweze kufanikiwa kimichezo ni lazima iwekeze kwa vijana kwenye michezo kwa gharama yoyote kwani kizuri ni gharama.
“Halmashauri zinapaswa kuhakikisha walimu wanapelekwa kwenye vyuo vya michezo na wanatumiwa ipasavyo na kuwe na viwanja vyenye ubora ili kuinua michezo nchini,” alisema Kairuki.
Aliwataka wazazi kutowakatisha tamaa watoto wao ambao wana vipaji vya michezo bali wawaunge mkono ili waweze kufikia mafanikio yao na nchi kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment