Friday, June 29, 2012

TUKIAMUA TUNAWEZA KUWEKEZA SUDANI KUSINI- MEJA GENERAL KISAMBA

Na Mwandishi Maalum,UN
Ushauri  umetolewa kwa Tanzania na Watanzania kuamka na   kuchangamkia fursa za uwekezaji na biashara ambazo zimejitokeza  nchini  Sudani ya Kusini.
Ushauri huo umetolewa siku ya Jumatano na Meja Jenerali Wynjones Kisamba,   Naibu Kamanda wa vikosi  vya kulinda amani  katika jimbo la Darfur   maarufu kama UNAMID,   wakati alipokutana na kubadilishana mawazo na maafisa wa Ubalozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, New York.
Meja Jenerali Kisamba  yuko hapa  Umoja wa Mataifa, kwa ziara ya kikazi na mafunzo  ya maafisa wa ngazi  za juu katika misheni za Umoja wa Mataifa, mafunzo ambayo yameandaliwa na Idara ya Operesheni za Ulinzi wa  Amani ya Umoja wa Mataifa (DPKO).
“ Tanzania tuna kila sababu ya kuwekeza nchini Sudani ya Kusini, zipo fursa nyingi mno kuanzia upelekaji wa chakula hadi ujenzi. Nilikuwa nyumbani hivi karibuni, nimekutana na viongozi mbalimbali na kuwaelezea juu ya fursa hizi”. Akasema Meja Jenerali
Na kuongeza.” Lakini wasiwasi wangu ni kwamba tunachelewa wakati majirani zetu wamekwisha zichangamkia fursa hizo na wako mbali sana sasa, kwa  maneno mengine naweza kusema wameishaingia mpaka jikoni” alisema Meja Jenerali huyo kwa hisia kubwa.
Aidha katika mazungumzo yake na maafisa wa ubalozi,  Naibu Kamanda wa vikozi vya UNAMID  amebainisha kwamba kama kweli serikali, kwa kushirikiana na  sekta za umma na binafsi zikiamua kuingia kibiashara   Sudani ya  Kusini hakuna tutakachopoteza.
“Sudani ya Kusini ndio kwanza wanaanza kuijenga nchi yao, wanachangamoto nyingi, sisi tunaweza kuwasaidia kwa maana ya kuwekeza na kwa kufanya biashara.  Kwa mfano wale wanakula sana chapati,  hawana ngano, tunaweza kuwauzia ngano, wanahitaji mafuta ya kupikia tunayo alizeti,  wanahitaji vifaa vya ujenzi, tuna viwanda vya saruji na nondo pia, kwa kweli fursa zipo tunachotakiwa ni kujipanga tu na kuwahamasisha wafanyabiashara wetu. Lakini kubwa na la msingi  zaidi, lazima Watanzania  tukubali  kuthubutu”. Amesisitiza Meja Jenerali Kisamba.
Akielezea  kuhusu suala zima la operesheni za kulinda amani   huko Darfur,   eneo ambalo yeye ni Naibu Kamanda akiongoza bataliani 17 zenye wanajeshi wapatao17,364 wakiwamo polisi 5,511 kutoka nchi 52,  Jenerali huyo alisema kuwa, kama ilivyo katika fursa za uwekezaji, Tanzania pia bado inayo fursa kubwa ya kujiimarisha  zaidi katika eneo la ulinzi wa amani.
Akaeleza kwamba, wanajeshi  kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)  pamoja na askari polisi wanaohudumu katika jimbo la Darfur wameonesha uhodari wa hali ya juu kiasi cha kupigiwa mfano na mataifa mengi makubwa.
“ Siyo kama najisifu, lakini watu wetu wameonesha uhodari na maarifa ya hali ya juu, wanafanya kazi nzuri, wanaheshimika,  wananidhamu, wanaitangaza vema Tanzania” akasema
Na kusisitiza. “Tumekuwa tukizungumzwa vizuri sana na baadhi wa washirika wetu kama vile Norway na  Sweden. Na hii inatupatia fursa ya  kujipanga vizuri zaidi kwa maana ya kuwaandaa na  kuongeza idadi ya wanajeshi na askari polisi katika eneo hilo”, akabainisha Jenerali Kisamba.
Kwa  mfano, akasema licha ya mahitaji makubwa ya wanajeshi, lakini kuna hitajio kubwa la askari polisi na hasa wanawake.
“ Tunahitaji  kuwekeza katika raslimali watu  kwa maana ya wanajeshi wetu na  polisi wetu. Wanajeshi wetu ni wazuri mno, na  polisi wetu ni wazuri pia, lakini,  na hasa kwa   polisi wetu  na kwa kuwa ndo wameanza karibuni. Hawa wanahitaji mafunzo zaidi katika ngazi ya kimataifa kutokana na ukweli kwamba mafunzo wanayopewa ni yale ya kukidhi mahitaji ya ndani ya nchi. Lakini ni kundi linahohitajika sana hivi sasa katika  operesheni za kulinda amani”. akasema
Aidha kwa kulitambua hilo, ameeleza kwamba  michakato mbalimbali inafanyika, ambayo pamoja  na mambo mengine, inahusisha kuwajengea uwezo na maarifa wanajeshi na polisi ili waweze kukidhi mahitaji na viwango vya kimataifa. Jambo litakalo rahisisha uwapo  na utayari   raslimali watu tayari kuhudu katika operesheni za kulinda amani  mara tu tunapoombwa na jumuia ya kimataifa kufanya hivyo.
Akizungumizia hali ilivyo  katika jimbo hilo la Darfur na maeneo mengine kwa ujumla, Meja Jenerali Kisamba amesema  kuwa, ingawa  wanajeshi wa kulinda amani wanajitahidi sana kutekeleza majukumu yao,   lakini  kusema ule ukweli hadi sasa hakuna amani ya kulinda jimboni Darfur.
Hata hivyo, akasema wanajeshi na polisi waliopo katika eneo hilo  wanaendelea kutekeleza majukumu yao, yakiwemo yale ya kulinda raia, jukumu ambalo linabaki kuwa kati ya majukumu makubwa kabisa ya UNAMID.
Kwa upande wake, Tanzania kwa sasa inacho kikosi kimoja cha kijeshi, kombania moja ya wahandisi wa medani, waangalizi wa amani na maafisa wanadhimu pamoja na polisi washauri. Ambao idadi yao yote kwa ujumla hadi kufikia mwezi Mei 2012 inafikia jumla 1,330.
Idadi hiyo inafanya nchi yetu kuwa katika nafasi ya 19 kidunia kati ya nchi 115 zitoazo walinzi wa amani chini ya Umoja wa Mataifa duniani. 

No comments:

Post a Comment

Idadi ya Wanaoperuzi Blogu hii